Monday, November 2, 2015

MSIMAMO MEDIA .COM: MSIMAMO MEDIA .COM: True value Media: SIMULIZI YA ...

MSIMAMO MEDIA .COM: MSIMAMO MEDIA .COM: True value Media: SIMULIZI YA ...:   True value Media: SIMULIZI ya



SIMU YA
MAMA…Sehemu ya2
Na Ismail Mang’ola

“NITARUDI MAMA YANGU” Yalikuwa ni maelezo mafupi ya kijana
Advocate Suma Mtata aliyoyaona huenda yangemfariji mama yake ili atakapokuwa
ameondoka asije akawa na kinyongo na mwisho wa siku mambo yakamwendea kombo.
Safari ya Advocate Suma Mtata imeanza, lakini haijulikani ni
wapi Advocate amedhamiria kwenda, kingine ni kwamba ameamua kuondoka bila hata
ya kuwaaga baadhi ya ndugu zake wa karibu hata marafiki zake waliotokea
kupendana sana.
Muda na masaa alioupoteza kijijini hapo aliona kama ilikuwa
ni mikosi kwake, licha ya kwamba kazi ya kilimo ilikuwa ikimpatia kipato na
hata wakati Vijana wengi walipokuwa wakihaha kwa kusaka pesa za kuwasaidia
kipindi cha kiangazi, yeye aliishi kama miongoni mwa watoto waliokuwa na maisha
ya kweli.
Sasa anaamua kuyaacha maisha hayo ya kilimo na kwenda kutafuta
maisha aliyoyaona yatakuwa na kipato kikubwa tofauti na hayo aliyokuwa
akiyategemea, hivyo aliamini huko anakoenda maisha yangekuwa mazuri zaidi ya
haya, akaondoka. Sasa endelea… *** Aliamini kwamba safari yake hiyo isingekuwa
ya maeneo ya karibu na mkoa wake alikotokea, dhamira ilikuwa ni kwenda kuishi
katika miji mikubwa moja ya miji hiyo ambayo aliiweka akilini mwake ni pamoja
na jiji la Dar es Salaam, Arusha na Jiji la Mwanza, maarufu ‘Rocky City.
Mbali na miji hiyo, pia aliutambua mji uliokuwa unaendelea
kukua kibiashara na kiuchumi mji wa Mbeya, huko Advocate Suma Mtata napo aliona
iwapo kama ataweza kuyazoea mazingira ya hali ya hewa, vilevile mawazo hayo
aliyaweka bayana kwenye akili yake.
Lakini hadi anaondoka kijijini hapo alikuwa bado hajapata
muafaka ni wapi anakokwenda na mji gani ambao ungeweza kumsaidia kuishi na
kufanya kazi ambayo itamuwezesha kupata kipato kikubwa zaidi ya kile alichokuwa
akikipata wakati akisahanya na kilimo.
Niukweli usiopingika kuwa, Advocate Suma Mtata alikuwa anapata
kipato kizuri katika harakati zake za kilimo. Labda alihitaji kubadilisha hali
ya upepo wa kipato hicho, kama tunavyojua, siku zote mwanadamu huwa haridhiki
na kile anachokipata, kwa kawaida ama kwa namna ninavyojua, unaweza kumpa
mshahara wa kutosha, lakini iwapo kama atasikia kuna sehemu wafanyakazi
wanalipwa juu ya ule anaolipwa kazini kwake, yuko tayari kwenda kufanyakazi
kwenye hiyo kampuni ambayo amesikia inalipa vizuri.
Hii ni kawaida kwa watanzania kufanya hivyo tena bila
kufikiria athari yake ni nini. Lakini ili mradi aachane na kipato hicho kidogo,
ndizo fikira za wengi wetu hapa nyumbani.
Majara ya saa nne Ikola anaenda nyumbani kwa kina Advocate
Suma Mtata, walikuwa na mipango yao ambayo walipanga jana yake kwa ajili ya
katika kijiji cha Ngamo kwa mjomba wake aambaye aliwaahidi angeenda
kuwatembelea baada ya kukutana mnadani.
“Mjomba usiwe na wasiwasi, nitakuja kuwatembeeni, hapa
katikati kuna vitu vilikuwa vimenibana sana mjomba, hivyo kwa sasa nahisi mambo
yameachia, kubwa naomba wasalimie nyumbani na uwahakikishie wiki hii nitakuja
kuwaona, najua ndugu zangu wamenikumbuka sana” Advocate Suma Mtata alimweleza
mjomba wake Mzee Hango kasha wakapeana mikono kwa minajili ya kuagana na
kuachana.
Ikola na Advocate Suma Mtata ni ndugu kwa upande wa mama zao,
mama yake na Advocate Suma ni mkubwa na mama yake na Ikola ni mdogo, wote
wamezaliwa tumbo moja na mzee Moghu.
Kwa hiyo walitambuana kuwa wote ni ndugu tena udugu wa ndani
kabisa. Lakini cha kushangaza, Ikola hakujua kama ndugu yake huyo, Advocate
Suma Mtata kama alikuwa na safari iliyokuwa imejificha, naamanisha hakumwambia
kama alikuwa anahitaji kusafiri siku za karibuni.
Pamoja na mipango hiyo ya kwenda Ngamu kwa mjomba Hango, bado
hakumweleza kama safari hiyo ilikuwa imeshaota mbawa, akamficha na mambo yake
yalipokuwa yamekamilika akalazimika kumuaga mama yake na dada yake Mwana pekee,
sio mabinamu zake wala wajomba wengine waliokuwa jirani na nyumbani kwao.
Majira ya saa kumi na mbili na robo, basi lililokuwa na namba
za usajili TZ 19171 lilifika katika stendi ya mabasi ya Kijota kisha akajitoma
ndani tayari kwa safari ya kuelekea katika mji mdogo wa Singida ambapo mwanzo
wa safari ya kuelekea miji mikubwa ndiko ilikokuwa inaanzia.
Basi alililopanda Advocate Suma Mtata ni basi ambalo lilikuwa
na sifa kubwa na kupelekea wanakijiji kulitungia nyimbo ambayo ilishika sana
hasa kwa wazee na Vijana waliokuwa wakinywa pombe za kienyeji.
Nakumbuka baada ya basi hilo kuwasili kwa mara ya kwanza
kijijini hapo, mbele liliandikwa ‘Singisa’ ambalo lilikuwa aina ya Layland,
lilikuwa na mlio mzuri sana, Vijana wengi waliupenda mlio wake na hata wakati
mwingine watu wengi waliweza kulitambua pale lilipokaribia kufika kijijini
likitokea mjini.
Lilikuwa na mngurumo wenye kusikika hata kama utakuwa mbali
kiasi gani, wengi waliweza kulitambua kuwa (Singisa inaingia) na kila lilipotua
kijijini hapo, Vijana kwa wazee na wale wa makamo waliweza kulishangilia na
kurukaruka utafikiri watoto wadogo, hali iliyoonyesha basi hilo lilipendwa
kupita maelezo ya kampuni iliyolitengeneza.
Kutoka kijijini hapo hadi mji mdogo wa Singida hapakuwa mbali
sana, ilikuwa ni umbali wa Maili moja, muda aliopanda basi hisi hilo kutoka
hapo hadi kufika mjini, lilitumia dakika sitini na tano kutokana na ubovu wa
miundombinu kipindi hicho ambapo barabara haikuwa nzuri, ilikuwa ni ya vumbi.
Hivyo mwendo wake usingeweza kuulinganisha na mwendo wa gari
linapokuwa kwenye barabara ya lami, ilikuwa ni shida sana kwa dereva kwenda
mwendo wa haraka, kwanza aliogopa kukata Springi, istoshe makorogesheni ya
ubovu huo wa barabara ilikuwa ni hatari kwa basi kuanguka hivyo ilibidi liende
mwendo wa kawaida.
Ikola alipofika nyumbani kwa mama yake mkubwa, alipoingia tu
ndani ya boma, aliuona mlango wa nyumba ya Advocate Suma Mtata ulikuwa
umefungwa na kufuli, akahisi labda atakuwa ameenda shambani kukata miwa, maana
wakati mwingine Advocate Suma Mtata alikuwa anapenda kwenda kushinda katika
shamba lao la miwa ambalo halikuwa mbali sana na hapo.
“Oooh mwanangu!!! Karibu baba” Mama yake na Advocate Suma
Mtata alimkaribisha Ikola mtoto wa mdogo wake, ‘Nyamaria’.
“Ahsante mama mkubwa, shikamoo mama” Ikola alimuamkia mama
yake mkubwa.
“Marhaaba mwanangu, Ikola! Habari za nyumbani” Mama
alimsalimia.
“Wote nyumbani hatujambo,mama sijui nyinyi huku”. Ikola
aliitikia na kisha naye akamrudishi salamu.
“Mwanangu huku hatujambo, ila kaka yako kaondoka!”
“Nani kaondoka?” Ikola alimuuliza mama yake mkubwa.
“Kaka yako Advocate Suma Mtata” akamjibu.
“Kaenda wapi?” Ikola akamuuliza tena.
“Mwanangu wee, hata haijulikani ni wapi ameenda, maana mimi
kaniambia kuwa amechoka kukaa hapa kijijini, hivyo ameona akatafute maisha huko
mijini, mwenyewe sijui kaenda mji gani ambako ameona atapata maisha mazuri”
Mama alimwelezea Ikola kwa kirefu kidogo.
“Inamaana hajakuambia ni wapi anaenda! Unataka kusema mama,
kajiondokea tu?” Ikola alimuuliza mama yake mkubwa kutaka kujua kwa undani zaidi.
“Kweli mwanangu, sijui hata moja zaidi ya pale aliponiambia
kuwa anataka kusafiri, na Habari ya safari yake kanieleza juzi jioni kashinda
jana na leo asubuhi nimeshangaa kuona mtu anagonga mlango wangu nilipoamka
nikamkuta ameshabeba bigi lake la nguo tayari kwa safari”. Mama aliendelea
kumweleza Ikola.
Mara kidogo akaingi Juma Shabani Nkumbi, Juma ni mtoto wa
kaka yake na Mama Advocate Suma Mtata wengi walipenda kumuita jina la mtoto
wake wa kwanza, anayeitwa ‘Mnyawi’ hivyo Bi. Mkubwa huyo akawa anaitwa kwa jina
hilo la mwanae wa kwanza ‘Nyamunyawi’ “Hodi” Juma alibisha hodi nyumbani kwa
shangazi yake”, baada ya kuingia ndani ya boma.
“Karibu mwanangu” Shangazi yake alimkaribisha.
“Shikamooo shangazi”. Juma alimuamkia shangazi yake Mama
Nyamunyawi.
“Mmeamkaje huku?” Juma alimsalimia shangazi yake.
“Sisi hatujambo mwanangu, nanyi hamjambo nyumbani?” Shangazi
yake naye akamrudishia salamu hiyo.
“Shangazi wote hawajambo” Juma naye akaipokea ile salamu na
kumjibu.
Baada ya salamu zile Juma aliamuulizia binamu yake Advocate
Suma Mtata kama alikuwepo wakati huo, alimiani kuwa alikuwa ndani kwa sababu
ilikuwa bado ni mapema hali ambayo asingekuwa na sehemu yeyote aliyeenda, kwani
kawaida vijijini iwapo kama mtu atakuwa ameenda mahali Fulani lazima wengi wao
watambue.
Hesabu ya wanavijiji hua inajulikana, kwanza ni uchache wa
wakazi pamoja na kutambuana kutokana na kila mkazi huonyesha upendo na
mshikamano wa kweli katika maisha yao hali ambayo inatofautiana na maisha ya
mijini.
“Mwanangu wee, mdogo wako hayupo! Kaondoka kwenda kutafuta
maisha huko alikoona atayapata”, Shangazi yake alimjibu.
“He! Kwani kaenda wapi?” Juma aliendelea kumuuliza shangazi
yake.
“Mwanangu hata najua basi, mwenyewe kasema atakapofika huko
safari yake itakapoishia ndipo atanijulisha kwa barua, lakini hadi anavuka
kizingiti hiki cha mlango hakuweza kuniambia ni wapi kaenda” Bi. Mkubwa huyo
alimweleza Juma mtoto wa kaka yake Mzee Shabani Nkumbi.
“Mhhhhh!” Juma alivuta pumzi na kimya cha sekunde kumi
kikafuata.
“Kwahiyo shangazi unataka kuniambia hajasema ni wapi anaenda!
Au kaenda Arusha? Maana siku nyingi alikuwa haachi kuahadithia mji wa Arusha”,
Juma aliendelea kumdadisi shangazi yake.
“Yaani mwanangu kukuambia ni wapi kaenda nitakuwa nmwenyewe
kasema akifika atakapoona hapo ndipo panamfaa ndipo atakapoandika barua na
kutujulisha ni wapi alipo lakini hadi anaondoka hapa, aliniacha nimeshika tama,
na hadi sasa namuwaza mwanangu, naona kama kaniacha mkiwa” Bi. Mkubwa
alioendelea kumjibu Juma.
“Shangazi acha mimi nirudi, maana kuna kazi nilitaka niifanye
pale nyumbani ya kufyetua matofali hivyo nilitaka nikasaidiane naye binamu
yangu, sasa kama hayupo ngoja nimfuate Munkulu kama nitamkuta?!” Juma alimjibu
shangazi na kisha akaaga na kuondoka.
Hali ile iliamsha upya mawazo kwa Bi. Mkubwa huyo namna ndugu
zake walivyokuwa hawakauki nyumbani hapo wakati Advocate Suma Mtata akiwepo,
Vijana wengi walipenda kumshirikisha katika kazi zao za kawaida kijijini hapo.


Hivyo Bi. Mkubwa alipomuona mtoto wa kaka yake kwenda
kumuulizia mwanae alihisi kama huko alikoenda ndio ulikuwa mwisho wa maisha
yake, lakini hakuwa na namna, Suma kashaondoka, kilichobaki ni kusubiri atarudi
ama ndio mwisho wake wa kuonana na ndugu zake hao.

MSIMAMO MEDIA .COM: True value Media: SIMULIZI YA SIMU YA MAMA

 True value Media: SIMULIZI YA SIMU YA MAMA: True value Media:  SIMU YA MAMA Na Ismail Mang’ola SIMU YA MAMA ni simulizi  inayomuhusu kijana Advocate Suma Mtata ambaye alitoweka ...

True value Media: SIMULIZI YA SIMU YA MAMA

True value Media: 

SIMU YA
MAMA
Na
Ismail Mang’ola
SIMU YA
MAMA

ni
simulizi  inayomuhusu kijana Advocate
Suma Mtata ambaye alitoweka nyumbani kwao miaka ishirini na tano iliyopita na
kuishia katika miji mikubwa na kusahau kurudi nyumbani.
Haikufahamika
kilichompelekea kuishia huko miji mikuu na kutokumbuka kama aliacha familia
yake huko kijijini kwao hali ambayo ilimlazimu mama yake  ahisi kuwa kijana wake labda alikuwa amezongwa
na starehe sambamba na wanawake ambao huwa chachu ya kuwasahaulisha baadhi ya
Vijana kutokumbuka makwao
. Ni simulizi yenye kuhuzunisha
iliyojaa mikasa mbalimbali ya kimaisha… Sasa unaweza kusonga nayo **** Sehemu
ya Kwanza ****
Alfajiri ya saa kumi na moja kasoro, kijana Addvocate Suma
Mtata anaamka na kuingia bafuni kwenda kuoga huku akionekana kuwa mtu mwenye
mawazo mengi sana kichwani mwake.
Haikuwa rahisi kumtambua kama alikuwa na mawazo kama
nilivyoweza kumtambua mimi mdogo wake ambaye mara nyingi chumba cha kulala
kilikuwa ni kimoja.
Maisha ya awali ya wanafamilia hiyo hayakuwa mabaya kihivyo,
wakati Advocate Suma Mtata alipokuwa anasoma elimu yake ya msingi hakuwa na
wazo hata kidogo ya kwenda kutafuta maisha mjini, aliamini kuwa maisha yake
yote angeyamalizia kwenye kazi za kilimo ambayo aliamini sana kuwa kilimo
kingeweza kumtoa kutokana na ukweli kwamba, alikuwa ni mkulima wa kweli na
aliweza kulima aina mbalimbali ya mazao.
Mazao aliyopendelea kulima wakati alipokuwa kijijini ni
Mahindi, mtama, ulezi, Alizeti na zao la kibiashara lililokuwa likimpatia fedha
mapema ni vitunguu, zao ambalo lilikuwa na upinzani mkubwa kwa wanavijiji.
Advocate Suma Mtata aliamini vitunguu ndio biashara iliyoweza
kumuingizia fedha mapema kabla ya mazao mengine aliyoweza kupanda na kuvuna,
hivyo aliizamishia akili yake kwenye mazao hayo ambayo ndiyo yalikuwa yakiuzika
mapema.
Lakini pia hakuacha kuzipa kipaumbele mazao mengine kama vile
Alizeti na ulezi ambavyo ndio mazao aliyoyageuza kuwa ni ya biashara wakati wa
kiangazi badala ya kuuza mahindi na mtama ambayo nayo alijiwekea uhakika kuwa
hayo ni kwa ajili ya chakula kipindi chote cha kiangazi na masika.
Baada ya kutoka bafuni, alirejea chumbani kwao na kuanza
kujiweka sawa kwa ajili ya maandalizi ya kuvaa nguo zake suruali aina ya Kadeti
nyeusi na Tirshirt nyeupe iliyokuwa na chengachenga nyeusi kwa nyeupe (mchemchele)
zilizoonekana kwa mbali na mara alipomaliza kazi hiyo akanyanyuka akaliendea begi
lake dogo la nguo kisha akaongozea kwenye mlango wa chumba cha Mama akagonga
ili amuage mama yake.
Lakini hata hivyo, Advocate suma Mtata alifikiria sana tena
kwa kina namna atakavyoweza kuyaamsha maisha mapya huko aendako, aliwafikiria
sana ndugu zake binamu ambao walikuwa bega kwa bega wakati wa kilimo ambapo
kawaida ilikuwa ikifikia labda ikiwa shamba lake limezidiwa na majani, hua kwa
kawaida hualika Kundi la Vijana kwa watu wa makamo na kupikwa pombe ya nguvu
kwa ajili ya walioalikwa kusaidia kilimo hicho.
Kwa kawaida wakulima iwapo kama hali hiyo itatokea ya
kuzidiwa na kilimo watu wengi vijijini huchukua kiasi cha debe nne za mtama na
kupikwa pombe kwa ajili ya watu hao watakaokuwa wamealikwa.
Pia huandaliwa Aidha mbuzi au majogoo wakubwa wanne, na kuchinjwa
pamoja na kupikwa ugali wa nguvu ambao 
utatosheleza zaidi ya watu ishirini lakini kubwa wafanyakazi ndio
wanaotakiwa kula na kushiba, yote hayo aliyawaza kabla ya kuanza safari
akiwafikiria ndugu zake ambao ndio waliokuwa washiriki katika harambee hiyo
nyakati za masika. 
Hakuna aliyejua kama Advocate Suma Mtata alikuwa na safari
yoyote ya kutoka nje ya kijiji hicho zaidi ya zile ambazo alikuwa akiagizwa na
mama yake labda kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya taarifa Fulani hasa mialiko
na misiba.
Siku hiyo haikuwa hivyo, hali ilikuwa nyingine, akanyanyuka
na kwenda kumuaga mama yake, “Ngongongo, ngongongo” aligonga mlango wa chumba
cha Bi. Mkubwa wake huku akiwa amesimama akiwa na dhamira ya dhati kumuaga mama
yake ili ajue wapi kijana wake kaenda.
“Nani”? Mama yake aliitika na kuuliza.
“Ni mimi mwanao mama” Advocate Suma Mtata alimjibu mama yake.
“Unasemaje usiku wote huu?” Mama Suma aliendelea kumuuliza.
“nataka nikuage mama yangu!”
“uniage!!!” Mama aliuliza kwa mshangao.
“Ndio mama, nataka kukuaga kuna sehemu nataka kwenda mara
moja”, alimjibu.
“Haya subiri nitoke” mama Suma alimjibu.
Mama Suma aliamka taratiibu na kisha akatoka na kumkuta
kijana wake akiwa amekaa kwenye kiti kidogo (kigoda) huku mikono yake miwili
ikiwa imekumbatia kidevu mithili ya mtu aliyekuwa akitafakari jambo.
“Haya! Mbona hivi?” mama alimuuliza Advocate Suma Mtata mtoto
wake wa mwisho aliyepelekea kumpenda kuliko watoto wake wengine.
“Mama, ukweli ni kwamba, maisha ya hapa kijijini kwangu
nimeona bora niyaage kwa muda Fulani, naenda kutafuta maisha mama, nimeangalia
namna ninavyoishi hapa kijijini hasa madharau ninayoangushiwa na hawa ndugu
zetu, mama nimeona sina sababu ya kuendelea kuishi hapa, sioni sababu ya
kubanana na watu ambao wanaonekana dhahiri hawapendi kuniona nikijishughulisha
na kilimo, ni mambo mengi sana wamekuwa wakinifanyia bila sababu ya msingi,
hivyo sina budi kuendelea kuwepo hapa mama yangu, kubwa niombee kwa mwenyezi
mungu kama nitafanikiwa mama nitarudi, hapa ni nyumbani kwetu na hakuna
aliyenifukuza, nimeona niepushe mambo mengine ambayo huenda yanaweza kutokea
katika maisha yetu haya Aidha inawezekana yakawa makubwa zaidi, tambua mama
humu duniani sio kila mtu atakupenda, kuna wapo ambao machoni ni wasafi lakini
moyoni sio” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake.
Kauli hiyo ya Advocate Suma Mtata kwa mama yake, haikuwa
nzuri na yenye kufariji, ilimhuzunisha sana mama yake hadi kupelekea Bi. Mkubwa
huyo kukaa kwenye benchi lililokuwa pale sebuleni naye akajikuta akisha tama
kwa kufikiria maneno aliyoyasema mwanae ya kutaka kuondoka kijijini hapo.
“Mwanangu! Lakini ujue kuwa wewe ndio ninayekutegemea hapa
nyumbani, sasa leo hii unataka kuondoka unafikiri nani atanisaidia kazi za hapa
nyumbani wakati mwenyewe unaniona hali yangu hii ya uzee?” Mama suma alimuuliza
mwanae kasha akaendelea kushika tama akisubiri mwanae amjibu.
“Mama, naomba usijali kuhusu hilo, nafikiri hawa wajukuu zako
Abdon na Muna watakusaidia, hawataweza kukuacha wakati wanajua fika hali yako,
kwanza Muna bado anasoma, ninaimani kubwa hawatakuacha, lakini kikubwa mama
barua zipo, nitakapofika huko ninakoenda, nitakujulisha kwenye barua kama
nimefika na nipo sehemu gani lakini kubwa hapa akili yangu kwanza nifike huko
ninakotaka kwenda” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake kisha akanyuka na
kusimama kwa ajili ya kuanza safari.
“Mwanangu hebu kaa kwanza, usiharakishe wakati mimi bado
sijakuelewa hata kidogo, huwezi kuniambia maneno ambayo hayaniingii akilini
kama unavyotaka wewe, huko unakoenda unakujua? Na ni nani atakupokea? Au
unajiendea tu mwanangu?” mama alimuuliza mwanae ili ajue anakokwenda.
“Mama nafikiri utataka kujua mengi kuhusiana na safari yangu
hii, safari hii si kwamba kuna mtu ananipeleka, nimeamua mwenyewe kuondoka na
nina imani huko ninakoenda nitafika salama wa salmini kwani elimu niliyokuwa
nayo si ya kunipoteza popote pale niendapo, nina akili, nina uwezo wa kufikiri
natambua baya na jema, hivyo mama yangu ondoa shaka na wala usije ukaingiwa na
hofu labda huko niendako nitaenda kubadilisha tabia niliyokuwa nayo, najua
kinachokufanya usononeke hivi ni kuhusu hilo, mama nakuhakikishia, kama
nitabadilika kitabia, hukuhuku ulipo naomba unilaani hadi niharibikiwe maisha
hayo ninayoenda kuyatafuta” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake kasha
akaonekana akishusha mikono yake kwenye shavu alipokuwa ameshika tama na
kumwambia’, “Nimekuelewa”.
“Nashukuru mama yangu kama utakuwa umenielewa” Advocate Suma
Mtata alimjibu mama yake kasha akakaa kimya kidogo akimsikilizia labda angekuwa
na lingine la kuongezea katika mazungumzo yao wakati ule.
“Kwa hiyo mama hapa ninaweza kuanza safari au bado mazungumzo
yanaendelea?” Advocate Suma Mtata alimuuliza mama yake.
Wakati huo muda uliokuwa ukisomeka kwenye saa ya Advocate
Suma Mtata saa aina ya Disco (Kimwekumweku) ilibainisha muda huo ulikuwa ni saa
kumi na moja na dakika 13, muda ambao mwenyewe Advocate Suma Mtata aliona kuwa
ulikuwa umemtupa mkono vibaya mno.
Advocate Suma Mtata hapo hakuwa na ujanja wa kuondoka iwapo
kama mama yake angegoma asiondoke, isingekuwa rahisi alazimishe safari hiyo
vinginevyo angedhurika mbele ya safari kabla ya kufika ama pindi atakapokuwa
anahanya na maisha ya huko mijini.
Hivyo ilibidi asubiri hadi dakika za mwisho atakapoisikia
kauli ya mama yake ikimruhusu, “Mwanangu Suma, natambua hii safari haina uzuri
kwako, na vilevile haya sio mawazo yako, hapa naona kuna kitu mwanangu, lakini
nisikuvunje moyo, nakupa Baraka zote huko uendako na mwenyezi Mungu
akutangulizie mikono yake ili akuongoze katika safari yako hiyo ili ufike
salama mwanangu, sitakuwa na la kusema, kwakuwa umeamua sasa mimi nitasemaje?”
Mama Suma alimalizia maneno yake ambayo yalionekana kumchoma Advocate Suma
Mtata ambaye alionekana akiinamisha uso wake sakafuni pia nikamuona akitoa
kitambaa chake mfukoni na kukipeleka katika paji lake la uso mithili ya mtu
aliyekuwa akifuta kitu Fulani hivi, hakikuwa kitu kingine yalikuwa ni machozi ambayo
yalitokana na usia aliokuwa akipewa na mama yake.
Pamoja na mama yake kumruhusu mwanae aende huko alikoona
kunaweza kumbadilisha kimaisha, hata hivyo muda wote huo Advocate Suma Mtata
hakuwa na uelewa wowote ni wapi angekwamia safari yake, pamoja na mama kuuliza
muda wote wa maongezi ni wapi alipokuwa amefikiria kwenda, lakini majibu ya
hapa na pale bado yalionekana kuwepo mbali, kiufupi hata yeye mwenyewe Advocate
Suma Mtata alikuwa hajui ni wapi safari yake ingeishia, akanyanyuka akamshika
mama yake mikono yote mawili, akamuaga kasha akamuaga dada yake aliyeitwa
Mwana, akatoka na kuanza safari.
Safari imeanza, lakini haijulikani ni wapi Advocate suma
Mtata anaenda, si yeye wala familia kujua ni wapi anaenda kutafuta maisha, je
ni nini kitafutia? Usikose kuifuatilia simulizi hii kali yenye kusisimua… Itaendelea.