Monday, November 2, 2015

True value Media: SIMULIZI YA SIMU YA MAMA

True value Media: 

SIMU YA
MAMA
Na
Ismail Mang’ola
SIMU YA
MAMA

ni
simulizi  inayomuhusu kijana Advocate
Suma Mtata ambaye alitoweka nyumbani kwao miaka ishirini na tano iliyopita na
kuishia katika miji mikubwa na kusahau kurudi nyumbani.
Haikufahamika
kilichompelekea kuishia huko miji mikuu na kutokumbuka kama aliacha familia
yake huko kijijini kwao hali ambayo ilimlazimu mama yake  ahisi kuwa kijana wake labda alikuwa amezongwa
na starehe sambamba na wanawake ambao huwa chachu ya kuwasahaulisha baadhi ya
Vijana kutokumbuka makwao
. Ni simulizi yenye kuhuzunisha
iliyojaa mikasa mbalimbali ya kimaisha… Sasa unaweza kusonga nayo **** Sehemu
ya Kwanza ****
Alfajiri ya saa kumi na moja kasoro, kijana Addvocate Suma
Mtata anaamka na kuingia bafuni kwenda kuoga huku akionekana kuwa mtu mwenye
mawazo mengi sana kichwani mwake.
Haikuwa rahisi kumtambua kama alikuwa na mawazo kama
nilivyoweza kumtambua mimi mdogo wake ambaye mara nyingi chumba cha kulala
kilikuwa ni kimoja.
Maisha ya awali ya wanafamilia hiyo hayakuwa mabaya kihivyo,
wakati Advocate Suma Mtata alipokuwa anasoma elimu yake ya msingi hakuwa na
wazo hata kidogo ya kwenda kutafuta maisha mjini, aliamini kuwa maisha yake
yote angeyamalizia kwenye kazi za kilimo ambayo aliamini sana kuwa kilimo
kingeweza kumtoa kutokana na ukweli kwamba, alikuwa ni mkulima wa kweli na
aliweza kulima aina mbalimbali ya mazao.
Mazao aliyopendelea kulima wakati alipokuwa kijijini ni
Mahindi, mtama, ulezi, Alizeti na zao la kibiashara lililokuwa likimpatia fedha
mapema ni vitunguu, zao ambalo lilikuwa na upinzani mkubwa kwa wanavijiji.
Advocate Suma Mtata aliamini vitunguu ndio biashara iliyoweza
kumuingizia fedha mapema kabla ya mazao mengine aliyoweza kupanda na kuvuna,
hivyo aliizamishia akili yake kwenye mazao hayo ambayo ndiyo yalikuwa yakiuzika
mapema.
Lakini pia hakuacha kuzipa kipaumbele mazao mengine kama vile
Alizeti na ulezi ambavyo ndio mazao aliyoyageuza kuwa ni ya biashara wakati wa
kiangazi badala ya kuuza mahindi na mtama ambayo nayo alijiwekea uhakika kuwa
hayo ni kwa ajili ya chakula kipindi chote cha kiangazi na masika.
Baada ya kutoka bafuni, alirejea chumbani kwao na kuanza
kujiweka sawa kwa ajili ya maandalizi ya kuvaa nguo zake suruali aina ya Kadeti
nyeusi na Tirshirt nyeupe iliyokuwa na chengachenga nyeusi kwa nyeupe (mchemchele)
zilizoonekana kwa mbali na mara alipomaliza kazi hiyo akanyanyuka akaliendea begi
lake dogo la nguo kisha akaongozea kwenye mlango wa chumba cha Mama akagonga
ili amuage mama yake.
Lakini hata hivyo, Advocate suma Mtata alifikiria sana tena
kwa kina namna atakavyoweza kuyaamsha maisha mapya huko aendako, aliwafikiria
sana ndugu zake binamu ambao walikuwa bega kwa bega wakati wa kilimo ambapo
kawaida ilikuwa ikifikia labda ikiwa shamba lake limezidiwa na majani, hua kwa
kawaida hualika Kundi la Vijana kwa watu wa makamo na kupikwa pombe ya nguvu
kwa ajili ya walioalikwa kusaidia kilimo hicho.
Kwa kawaida wakulima iwapo kama hali hiyo itatokea ya
kuzidiwa na kilimo watu wengi vijijini huchukua kiasi cha debe nne za mtama na
kupikwa pombe kwa ajili ya watu hao watakaokuwa wamealikwa.
Pia huandaliwa Aidha mbuzi au majogoo wakubwa wanne, na kuchinjwa
pamoja na kupikwa ugali wa nguvu ambao 
utatosheleza zaidi ya watu ishirini lakini kubwa wafanyakazi ndio
wanaotakiwa kula na kushiba, yote hayo aliyawaza kabla ya kuanza safari
akiwafikiria ndugu zake ambao ndio waliokuwa washiriki katika harambee hiyo
nyakati za masika. 
Hakuna aliyejua kama Advocate Suma Mtata alikuwa na safari
yoyote ya kutoka nje ya kijiji hicho zaidi ya zile ambazo alikuwa akiagizwa na
mama yake labda kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya taarifa Fulani hasa mialiko
na misiba.
Siku hiyo haikuwa hivyo, hali ilikuwa nyingine, akanyanyuka
na kwenda kumuaga mama yake, “Ngongongo, ngongongo” aligonga mlango wa chumba
cha Bi. Mkubwa wake huku akiwa amesimama akiwa na dhamira ya dhati kumuaga mama
yake ili ajue wapi kijana wake kaenda.
“Nani”? Mama yake aliitika na kuuliza.
“Ni mimi mwanao mama” Advocate Suma Mtata alimjibu mama yake.
“Unasemaje usiku wote huu?” Mama Suma aliendelea kumuuliza.
“nataka nikuage mama yangu!”
“uniage!!!” Mama aliuliza kwa mshangao.
“Ndio mama, nataka kukuaga kuna sehemu nataka kwenda mara
moja”, alimjibu.
“Haya subiri nitoke” mama Suma alimjibu.
Mama Suma aliamka taratiibu na kisha akatoka na kumkuta
kijana wake akiwa amekaa kwenye kiti kidogo (kigoda) huku mikono yake miwili
ikiwa imekumbatia kidevu mithili ya mtu aliyekuwa akitafakari jambo.
“Haya! Mbona hivi?” mama alimuuliza Advocate Suma Mtata mtoto
wake wa mwisho aliyepelekea kumpenda kuliko watoto wake wengine.
“Mama, ukweli ni kwamba, maisha ya hapa kijijini kwangu
nimeona bora niyaage kwa muda Fulani, naenda kutafuta maisha mama, nimeangalia
namna ninavyoishi hapa kijijini hasa madharau ninayoangushiwa na hawa ndugu
zetu, mama nimeona sina sababu ya kuendelea kuishi hapa, sioni sababu ya
kubanana na watu ambao wanaonekana dhahiri hawapendi kuniona nikijishughulisha
na kilimo, ni mambo mengi sana wamekuwa wakinifanyia bila sababu ya msingi,
hivyo sina budi kuendelea kuwepo hapa mama yangu, kubwa niombee kwa mwenyezi
mungu kama nitafanikiwa mama nitarudi, hapa ni nyumbani kwetu na hakuna
aliyenifukuza, nimeona niepushe mambo mengine ambayo huenda yanaweza kutokea
katika maisha yetu haya Aidha inawezekana yakawa makubwa zaidi, tambua mama
humu duniani sio kila mtu atakupenda, kuna wapo ambao machoni ni wasafi lakini
moyoni sio” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake.
Kauli hiyo ya Advocate Suma Mtata kwa mama yake, haikuwa
nzuri na yenye kufariji, ilimhuzunisha sana mama yake hadi kupelekea Bi. Mkubwa
huyo kukaa kwenye benchi lililokuwa pale sebuleni naye akajikuta akisha tama
kwa kufikiria maneno aliyoyasema mwanae ya kutaka kuondoka kijijini hapo.
“Mwanangu! Lakini ujue kuwa wewe ndio ninayekutegemea hapa
nyumbani, sasa leo hii unataka kuondoka unafikiri nani atanisaidia kazi za hapa
nyumbani wakati mwenyewe unaniona hali yangu hii ya uzee?” Mama suma alimuuliza
mwanae kasha akaendelea kushika tama akisubiri mwanae amjibu.
“Mama, naomba usijali kuhusu hilo, nafikiri hawa wajukuu zako
Abdon na Muna watakusaidia, hawataweza kukuacha wakati wanajua fika hali yako,
kwanza Muna bado anasoma, ninaimani kubwa hawatakuacha, lakini kikubwa mama
barua zipo, nitakapofika huko ninakoenda, nitakujulisha kwenye barua kama
nimefika na nipo sehemu gani lakini kubwa hapa akili yangu kwanza nifike huko
ninakotaka kwenda” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake kisha akanyuka na
kusimama kwa ajili ya kuanza safari.
“Mwanangu hebu kaa kwanza, usiharakishe wakati mimi bado
sijakuelewa hata kidogo, huwezi kuniambia maneno ambayo hayaniingii akilini
kama unavyotaka wewe, huko unakoenda unakujua? Na ni nani atakupokea? Au
unajiendea tu mwanangu?” mama alimuuliza mwanae ili ajue anakokwenda.
“Mama nafikiri utataka kujua mengi kuhusiana na safari yangu
hii, safari hii si kwamba kuna mtu ananipeleka, nimeamua mwenyewe kuondoka na
nina imani huko ninakoenda nitafika salama wa salmini kwani elimu niliyokuwa
nayo si ya kunipoteza popote pale niendapo, nina akili, nina uwezo wa kufikiri
natambua baya na jema, hivyo mama yangu ondoa shaka na wala usije ukaingiwa na
hofu labda huko niendako nitaenda kubadilisha tabia niliyokuwa nayo, najua
kinachokufanya usononeke hivi ni kuhusu hilo, mama nakuhakikishia, kama
nitabadilika kitabia, hukuhuku ulipo naomba unilaani hadi niharibikiwe maisha
hayo ninayoenda kuyatafuta” Advocate Suma Mtata alimweleza mama yake kasha
akaonekana akishusha mikono yake kwenye shavu alipokuwa ameshika tama na
kumwambia’, “Nimekuelewa”.
“Nashukuru mama yangu kama utakuwa umenielewa” Advocate Suma
Mtata alimjibu mama yake kasha akakaa kimya kidogo akimsikilizia labda angekuwa
na lingine la kuongezea katika mazungumzo yao wakati ule.
“Kwa hiyo mama hapa ninaweza kuanza safari au bado mazungumzo
yanaendelea?” Advocate Suma Mtata alimuuliza mama yake.
Wakati huo muda uliokuwa ukisomeka kwenye saa ya Advocate
Suma Mtata saa aina ya Disco (Kimwekumweku) ilibainisha muda huo ulikuwa ni saa
kumi na moja na dakika 13, muda ambao mwenyewe Advocate Suma Mtata aliona kuwa
ulikuwa umemtupa mkono vibaya mno.
Advocate Suma Mtata hapo hakuwa na ujanja wa kuondoka iwapo
kama mama yake angegoma asiondoke, isingekuwa rahisi alazimishe safari hiyo
vinginevyo angedhurika mbele ya safari kabla ya kufika ama pindi atakapokuwa
anahanya na maisha ya huko mijini.
Hivyo ilibidi asubiri hadi dakika za mwisho atakapoisikia
kauli ya mama yake ikimruhusu, “Mwanangu Suma, natambua hii safari haina uzuri
kwako, na vilevile haya sio mawazo yako, hapa naona kuna kitu mwanangu, lakini
nisikuvunje moyo, nakupa Baraka zote huko uendako na mwenyezi Mungu
akutangulizie mikono yake ili akuongoze katika safari yako hiyo ili ufike
salama mwanangu, sitakuwa na la kusema, kwakuwa umeamua sasa mimi nitasemaje?”
Mama Suma alimalizia maneno yake ambayo yalionekana kumchoma Advocate Suma
Mtata ambaye alionekana akiinamisha uso wake sakafuni pia nikamuona akitoa
kitambaa chake mfukoni na kukipeleka katika paji lake la uso mithili ya mtu
aliyekuwa akifuta kitu Fulani hivi, hakikuwa kitu kingine yalikuwa ni machozi ambayo
yalitokana na usia aliokuwa akipewa na mama yake.
Pamoja na mama yake kumruhusu mwanae aende huko alikoona
kunaweza kumbadilisha kimaisha, hata hivyo muda wote huo Advocate Suma Mtata
hakuwa na uelewa wowote ni wapi angekwamia safari yake, pamoja na mama kuuliza
muda wote wa maongezi ni wapi alipokuwa amefikiria kwenda, lakini majibu ya
hapa na pale bado yalionekana kuwepo mbali, kiufupi hata yeye mwenyewe Advocate
Suma Mtata alikuwa hajui ni wapi safari yake ingeishia, akanyanyuka akamshika
mama yake mikono yote mawili, akamuaga kasha akamuaga dada yake aliyeitwa
Mwana, akatoka na kuanza safari.
Safari imeanza, lakini haijulikani ni wapi Advocate suma
Mtata anaenda, si yeye wala familia kujua ni wapi anaenda kutafuta maisha, je
ni nini kitafutia? Usikose kuifuatilia simulizi hii kali yenye kusisimua… Itaendelea.
     

No comments:

Post a Comment