Saturday, June 2, 2012

JINA LA KUITWA USTADHI LAMKERA MAKAMBA

Na Ismail Mang'ola

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Luteni mstaafu Yusuf Rajabu Makamba, amesema imefikia wakati naye aitwe sheikh badala ya hivi sasa anavyoitwa Ustadhi kutokana na mambo mengi ambayo amekuwa akiyafanya hasa yale yanayowahusu Masheikh.

 Bw. Makamba ameyabainisha hayo mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Karimjee wakati wa uzinduzi wa vitabu vyake BINADAMU NA KAZI na kile kinachokwenda kwa jina la UKWELI KWA MUJIBU WA BIBILIA NA KURU'AN TUKUFU ambavyo vilizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Ghalib Bilal huku viongozi wengine wakihudhuria.

Kiongozi huyo alisema kwamba, hivi sasa kuna ulazima wa kuitwa Sheikh na sio Ustadhi tena kwa kuwa tayari ameshafanya mambo ambayo yalipaswa kufanywa na masheikhn kwa kutunga vitabu ambavyo vinahusisha makatazo ya kupokea na kutoa rushwa.

Aliendelea kuueleza uma uliofurika ukumbini hapo na kusema kwamba, kutokana na kuona jamii inazidi kupotoka na mambo mbalimbali yasiyokuwa na mafundisho, hivyo alilazimika kuingilia kati kazi za masheikh hao pamoja na maaskofu kuandika vitabu hivyo ambavyo hivi sasa wizara ya Elimu na Ufundi imeridhia wanafunzi wa darasa la tano (V) na la saba (VII) kujifunza mambo kadha wa kadha kupitia vitabu hivyo hasa kile cha BINADAMU NA KAZI.

Makamba alisema, awali vitabu hivyo vilizinduliwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa tanzania Fredrick Sumaye, lakini tangu hapo vilikuwa bado havijaanza kutumika rasmi lakini siku za hivi karibuni alifanya kila liwezekanalo ili vitabu hivyo vianze kutumika hasa mashuleni kwa ajili ya kuwapatia vijana wetu wanafunzi upeo na ufahamu kaatika mambo mbalimbali yaliyomo ndani ya vitabu hivyo.

 Mhe. Makamba alisema hivi sasa mwanadamu anatakiwa kufanya kazi kwa bidii zote ili kuleta mabadiliko kuliko kukaa na kucheza michezo ambayo haina mantiki na wala haitaweza kuwaletea faida yeyote katika maisha ya sasa, alisema na ndio maana watu wanamuona kila wakati anakuwa mkali, ukali huo unatokana na kuona watu wengi huwa hawapendi kujishughulisha na ndio maana anafikia hatua ya kuwakemea hata kama hawafahamiani kwa ukaribu.

Alikumbushia hata kipindi alipokuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaama, alisema alishawahi kufunga baa zote hapa mjini zile ambazo zilikuwa zikifunguliwa kuanzia asubuhi hadi usiku, alisema watu wengi walikuwa hawaendi makazini na badala yake wanashinda baa kwa kunywa kitu ambacho alikielezea kuwa huo ni uzembe na uvivu, alisema Luteni mstaafu Makamba.

Makamba alisema hivi sasa pamoja na kustaafu, lakini bado anajishughulisha ambapo kazi yake kubwa ni mfugaji wa Ng'ombe pamoja na kilimo huku mkewe akijishughulisha na ufugaji wa kuku, alisema Katibu huyo mstaafu. 

No comments:

Post a Comment